Jaji Mkuu Martha Koome amesema idara ya mahakama inatambua juhudi zinazopigwa na mfumo mbadala wa kutatua mizozo miongoni mwa jamii zinazoishi Kaskazini Mashariki kwa kufanyia haki wanyonge na kupunguza uhasama na chuki miongoni mwao. Akizungumza wakati alipofungua rasmi kituo cha mfumo huo katika mahakama kuu ya Garissa, Koome alisema maadili ya usawa lazima yazingatiwe wakati wa kutoa haki kwa wahusika kupitia mfumo huo. Aidha viongozi wa kaunti hiyo walikumbatia mfumo huo wakisema utapunguza muda wa kuamua kesi zinazochipuka hasa migorogoro ya ardhi, sehemu za lishe na maji, maswala ya urithi miongoni mwa mengine bila kugharamika kufika mahakani kila wakati kusikiza kesi hizo.