Baadhi ya vijana katika kaunti ya Nyamira wameshiriki maandamano ya amani mjini Nyamira, kulalamikia kukithiri kwa visa vya ufisadi miongoni mwa maafisa wa serikali ya kaunti hiyo.
Hii ni baada ya waziri wa fedha nchini John Mbadi kusitisha matumizi ya mamilioni ya pesa za benki ya dunia kwenye kaunti hiyo, kutokana na matumizi yasiyoeleweka ya zaidi ya shilingi milioni 20 zilizolenga kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo. Wakiwahutubia wanahabari katika eneo la Konate viungani mwa mji wa Nyamira, vijana hao wamemtuhumu gavana Amos Nyaribo kwa madai ya kuhusika kwenye ufisadi na kumtaka kujiuzulu ili kutoa fursa kwa uchunguzi huru na kweli.