
89 views
STORY 1.. UPASUAJI SHAKAHOLA Shughuli ya kuifanyia upasuaji mili zaidi iliyopatikana katika Msitu wa Shakahola kwenye Kaunti ya Kilifi inatarajiwa kuanza leo hii katika Hifadhi ya Maiti ya Kaunti Ndogo ya Malindi. Upasuaji wa mili hiyo ni wa awamu ya pili baada ya hapo awali mili mingine 112 kufanyiwa upasuaji. Shughuli hiyo ya leo inatarajiwa kuendelea sambamba na ile ya kuitambua mili ambayo tayari imefukuliwa. Kufikia sasa idadi jumla ya watu ambao hawajulikani waliko ni 613, mtu mmoja zaidi aliokolewa hapo jana na kufikisha 91 idadi ya waliookolewa, waliotambuliuwa na jama zao ni 19 huku waliokamatwa wakiwa 34. Shughuli ya kuifukua mili zaidi inatarajiwa kuendelea baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ya upasuaji. Ikumbukwe upasuaji wa mili kufikia sasa umebainisha kwamba baadhi ya watu hao ambao walikuwa wafuasi wa Mhubiri Paul Makenzie walifariki dunia kwa kujinyima chakula, kuuliwa kwa kupigwa kwa vifaa butu kichwani, kunyongwa vilevile kuzibwa pua na midomo ili kuwazuia kupumua hadi kufariki dunia. STORY 2..KAMATI KUH KODI Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Kadri, KUPPET ni miongoni mwa vyama ambavyo leo ni zamu yao ya kuwasilisha maoni kuhusu kodi zinazopendekezwa katika Mswada wa Kifedha wa Mwaka 2023. Hapo jana ilikuwa zamu ya Chama cha Watengenezaji wa Bidhaa, KAM na Sekta ya Binafsi,KEPSA kuwasilisha maoni yao ambapo pande hizi zilionya kuhusu uwezekano wa watu elfu mia moja kukoseshwa ajira endapo mapendekezo ya mswada huo yatatekelezwa. KEPSA aidha imeonya kwamba huenda Kenya ikapoteza shilingi bilioni 150 iwapo kampuni mbalimbali zitaendelea kujiondoa humu nchini kufuatia kupanda kwa gharama ya uwekezaji. Kampuni hizo zinahofiwa kutozwa kodi maradufu endapo mswada huo utapitishwa. Lakini unafahamu ni kwanini Kamati hiyo inaendelea kupokea maoni ya wananchi kuhusu Mswada huo wa Fedha wa mwaka 2023? Katika nukuu ya Sheria ya Mwaka 2019 kuhusu kuhusishwa kwa umma inasema kwamba. Ni hitaji la kisheria kwa Bunge la Kitaifa na Seneti kutoa nafasi kwa umma kuwasilisha maoni yake kuhusu masuala mbalimbali yanayoshughulikiwa na mabunge hayo. Mwananchi anaweza kuwasilisha maoni hayo kupitia waraka ama kujiwasilisha mwenyewe mbele ya kamati na kutoa maoni yake. Iwapo Mkenya ama mashirika yatakosa kupata fursa ya kuwasilisha maoni, yana haki ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mchakato mzima wa suala ambalo hawakuhusishwa. STORY 3…VITISHO AZIMIO Mrengo wa Azimio utatoa mwelekeo Jumanne wiki ijayo kuhusu mazungumzo baina yake na serikali kupitia kamati ya pamoja. Azimio imetoa makataa ya siku sita ya kusuluhishwa kwa masuala mbalimbali la sivyo mazungumzo baina yake na serikali yafutiliwe mbali kabisa. Miongoni mwa masuala ambayo Azimio inataka yashughulikiwe mara moja ni kupunguzwa kwa gharama ya maisha, kukaguliwa kwa sava zilizotumika kuhifadhi matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, kufanywa kwa mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi, IEBC vilevile kutokuwa na miingilio kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza katika vyama tanzu vya Azimio hasa Jubilee. Eugene Wamalwa ambaye ni mmoja wa viongozi wa Azimio aliyasoma masharti hayo hapo jana wakati wa kikao na wanahabari ambacho pia kilihudhuria na vinara wengine wa Azimio wakiwamo Raila Odinga, Martha Karua na Kalonzo Musyoka. Azimio aidha imemtaka Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu kujiujzulu wadhifa wake kwa madai ya kuruhusu kutumiwa na serikali ili kusambaratisha uongozi wa chama hicho. Hata hivo Nderitu amejitetea kutokana na tangazo lake la kuidhinisha kutimuliwa katika uongozi wa Chama cha Jubilee kwa Katibu Mkuu wa Chama, Jeremiah Kioni, Naibu Mwenyekiti David Murathe vile vile mweka hazina. Nderitu hata hivyo amesema kwamba viongozi wa chama hicho wana nafasi ya kutatua mzozo uliopo huku Jopo la Kusuluhisha Mizozo ya Vyama vya Kisiasa likiratibu Mei 31 kuwa ya kikao cha kushughulikia malalamishi yaliyoibuliwa kuhusu mchakato wa kuwaondoa viongozi wengine chamani. CONNECT WITH US: https://linktr.ee/radio47 SMS line: 24047 Calls: 0793047047 WhatsApp: 0719739487