
14,267 views
Nyote mwakumbuka wakti msanii chipukizi wa nyimbo za injili humu nchini, Kevin Kioko anayejulikana kama 'Bahati' alipokosa kufika katika studio zetu pindi tu aliposhangaza dunia huku wengi wakijawa na mihemko tele, baada ya kuketi katika kiti cha rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto. Hayo yote yalitendeka katika sherehe za uzinduzi rasmi wa chama cha Jubilee uwanjani Kasarani. Wiki moja baadae alialikwa na watangazaji Gidi na Ghost katika kitengo cha waliobobea lakini alichelewa huku akilaumu msongamano wa magari na kuahidi kurudi tena kabla ya mwaka huu kufika tamati. Basi miezi kadhaa baadae, msanii huyu maarufu ajulikanae kwa nyimbo kama 'Mama' 'Barua' na 'Kuchu Kuchu' alitimiza ahadi yake na kutembelea studio zetu siku ya Ijumaa, 16/12/2016. Katika mahojiano yake ya kusisimua na mtangazaji Ghost, Bahati alizungumzia mengi lakini aliwafurahisha wasikilizaji wengi wa Radio Jambo haswa kina dada alipofichua kuwa bado hajafanikiwa kupata jiko na kuwa yuko katika pilkapilka za kupata mke. Bahati alifichua hayo baada ya mashabiki wake kutaka kujua kama ameoa au ana mchumba, swali ambalo liliulizwa hii leo na shabiki mmoja. "Hilo ndilo swali nlilokuwa nimesubiri. Nateseka sana, nateseka sana sina bibi hata sina uchumba na yeyote tafadhali mtu ajitokeze anisaidie." Alijibu msanii huyo.