
1,396 views
Wiki iliyopita, mojawapo ya mambo yaliyogonga vichwa vya habari na pia vichwa au nyuso za watu (lengo lake ucheshi tu) ni tukio lililomhusisha gavana wa kaunti ya Bomet, mheshimiwa Isaac Rutto ambapo pamoja na wafuasi wake walitupiwa vitoa machozi huku akiumizwa usoni katika pilkapilka hizo. Haya yalitokea wakti ambapo mzozo ulitokea katika maeneo ya Silibwet kaunti ya Bomet katika kinyang'anyiro cha kadanda kati ya bunge fc na silbwet fc, ambapo wafuasi wa mheshimiwa Joyce Laboso walitofautiana na wafuasi wake Rutto jambo lililozua mtafaruku. Gavana Rutto alilazimika kutafuta matibabu Nairobi huku akidai kuwa alishambuliwa na polisi na siku moja baadaye, ilimlazimu asafiri hadi Afrika Kusini kutafuta matibabu zaidi. Lakini je ni lipi haswa lililotokea?. Naibu wa spika wa binge, bi Joyce Laboso alikuwa studioni hii leo kuangazia mambo ya kisiasa na swala hilo kama ilivyotarajiwa lilitokea na hakuwa na budi ila kuweka kila mtu sawa ni yepi haswa yaliyotokea. "Kwa ufupi ningependa gavana wetu aende aandikishe taarifa kwa polisi huku akilalamika kirasmi ili uchunguzi ufanywe. Jinsi ya kujua ukweli wa mambo ni uchunguzi ufanywe ili kila mtu ajue. Ukweli ulio mezani ni kuwa nilikuwa katika shughuli zangu, yeye akaja kwa shughuli zangu na wafuasi wake ikaleta mvutano kati ya wafuasi wake na wangu." Alifafanua bi Laboso ambaye ndiye alikuwa amedhamini mashindano hayo ya kadanda. Kando na hayo, bi Laboso alielezea nia yake ya kumng'atua bwana Rutto katika kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu ujao na juhudi alizonazo a kuleta wananchi wote pamoja, haswa katika maeneo ya bonde la ufa.