
306 views
Wakati wa kipindi cha jana cha #MazungumzoWaziWazi, Eudias Kigai alizungumza na msikilizaji mmoja wa Radio Jambo kutoka Nakuru aliyemsimulia kisa cha kushangaza na kuchekesha sana. Msikilizaji huyo ambaye anajulikana kama Wilson alieleza Eudias kuwa rafikiye ambaye alimtaja kwa jina, Aoko, ana uraibu wa kuvuta bangi na jambo hilo humsababisha kufanya vitu vya kushangaza na kuchekesha si haba. Katika siku za hivi karibuni, Wilson alidai kuwa Aoko alimpiga mkewe katika hali ya kutatanisha sana. Wilson alisema kuwa baada ya kuvuta bangi, Aoko alienda nyumbani ambapo aliomba mkewe ampatie maji ya kunywa. Bibiye alitii ombi lake na akamletea maji katika bilauri. Muda mchache baada ya hiyo, mume alimrukia na kuanza kumpiga huku akidai amweleze ni nini alichokuwa anafanya na Mhubiri Victor Kanyari wakiwa wameshikana mikono. Aoko alidai kuwa amewaona ndani ya bilauri wakiwa wameshikana mikono na alitaka amweleze mbona anafanya hivyo. Ikiwa kuna kisa ambacho kinadhibitisha kuwa bangi ni mbaya basi ni hiki.