Shughuli za biashara zimetatizwa mjini Mbale, kaunti ya Vihiga, baada ya mamia ya wakazi kuandamana wakilalamikia ubakaji na mauaji ya mtoto wa darasa la tisa. Waandamanaji hao, wakiwemo wanaharakati, walitembea kwa takribani kilomita tano hadi afisi ya kamishna wa kaunti huku wakiwa wamebeba jeneza na mabango wakitaka haki itendeke. Hata hivyo, walizuiwa na polisi na kushindwa kuingia katika afisi hiyo. Mamake mtoto huyo amesema bintiye alitoweka Jumatatu iliyopita na baadaye mwili wake kupatikana Jumanne, ambapo inadaiwa alinyongwa. Waandamanaji wamelalamikia ongezeko la visa vya ubakaji na mauaji katika eneo hilo na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kuzuia matukio kama hayo kujirudia.