Timu za Migori Youth na Mombasa United zimepata ushindi wa bao 1-0 mwishoni mwa wiki na kusalia kileleni mwa Ligi ya Daraja la Pili (NSL), huku zikiwa zimesalia mechi nne msimu kukamilika. Migori Youth na Mombasa United wote wana alama 71 kileleni mwa ligi, huku 3K FC ikiifuata katika nafasi ya tatu kwa alama 69.
3K FC ilipoteza pointi muhimu nyumbani baada ya kutoka sare tasa na Benki ya Equity FC. Kulingana na ratiba, 3K FC itamenyana na Mombasa United nyumbani Jumatano kabla ya kukutana na Talanta katika mechi inayofuata.
Kwa upande wa Mombasa United, baada ya mechi hiyo dhidi ya 3K FC, itasafiri kwenda Bungoma kucheza na Nzoia kabla ya kumenyana na Luanda Villa na Naivas katika mechi mbili za mwisho.
Viongozi Migori Youth wanacheza na MCF nyumbani kabla ya mechi tatu ngumu dhidi ya Kisumu All Stars, Equity FC na 3K FC. Timu tatu bora mwishoni mwa msimu zinatarajiwa kupandishwa daraja hadi Ligi Kuu msimu ujao.