Idara ya Hali ya Hewa imethibitisha kuanza mapema kwa mvua ya masika katika maeneo ya Nairobi, magharibi, kati na nyanda za juu, huku maeneo ya kaskazini na pwani yakitarajiwa kupata mvua baadaye, kati ya mwishoni mwa Machi na katikati ya Aprili.
Hata hivyo, kutokana na mvua za muda mfupi zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya nchi, wakulima wamechanganyikiwa kwa vile hawana uhakika wa kupanda mbegu au kusubiri. Katika Kaunti ya Nyandarua, wakulima wengi tayari wametayarisha mashamba yao kwa ajili ya upanzi lakini hawana uhakika kama mvua inayonyesha itaendelea hadi msimu ukamilike.