Serikali yatoa wito kwa hospitali binafsi kupunguza gharama za matibabu ya figo

  • | VOA Swahili
    235 views
    Serikali na hospitali binafsi nchini Tanzania zimetakiwa kutafuta njia za kupunguza gharama za matibabu ya figo na kuboresha huduma za Afya kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu hayo. Wakizungumza na Sauti ya Amerika baadi ya Wagonjwa na wadau wa afya wametoa wito huo kuhakikisha wagonjwa wa figo wanapata matibabu na kishauri matibabu hayo kuingizwa kwenye mfuko wa bima ya Afya. Mariamu Mapinda ni mzaliwa wa Bariadi ambae ana tatizo la figo kwa kipindi cha muda mrefu ambalo limemfanya apate changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo kuvimba baadhi ya sehemu za mwili, mifupa kuishiwa nguvu pamoja na shinikizo la damu la mara kwa mara. Mbali na kupata mtu wa kujitolea fogo, lakini gharama za upandikizaji pamoja na vipimo zimekuwa vikwazo vikubwa katika kufanikisha upandikizaji huo. “ili niweze kurudi katika hali yangu na changamoto ninazopitia natakiwa kupandikiziwa figo lakini kuna gharama ambazo natakiwa kulipia. waliniambia kupandikiza figo gharama yake ni Millioni thelathini na vipimo kwa mtoaji figo itahitajika pesa nyengine” amesema Mapinda. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 9.1 mpaka asilimia 13.1 ya watu duniani wanaishi na magonjwa mbalimbali ya figo, kwa upande wa Tanzania asilimia 7 ya watu wanaoishi vijijini wanaishi na magonjwa ya figo na asilimia 15.5 ya watu wanaoishi mijini wanaishi na magonjwa mbalimbali ya figo. Asia Mustapha kutoka Dar es Salaam ni mgonjwa wa figo na hapa anaeleza changamoto ambazo amekuwa akipitia ikiwemo dawa kuuzwa kwa bei kubwa na baadhi ya dawa hizo hazipatikani ndani ya nchi na kulazimika ziagizwe kutoka nje ya nchi. Amesema “bei ya dawa zipo juu na vile vile kuna dawa nyingi ambazo hazipatikaniki. mfano hai ni mimi mwenyewe natakiwa kutumia dawa za kupandisha presha mimi presha yangu ni ya kushuka lakini dawa ya kupandisha presha haipatikani hivyo lazima niagize kutoka india kwahiyo wangapi wanaweza kuagiza kutoka nje. Akizungumzia gharama za matibabu Dkt Saidi Kanenda ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka hospitali ya Bugando mkoani Mwanza amesema gharama kubwa ya matibabu ya figo hii yanatokana na vifaa vingi vinavyotumika kuagizwa kutoka nje ya nchi. “Gharama ni kubwa na huwezi kumudu kwasababu huku kwetu hatutengenezi hivi vifaa kwahiyo tunategemea vifaa vya kununua kutoka nje ya nchi na hivyo vifaa vingine vinavyotumika vinatoka nje ya nchi na gharama yake ni kubwa” alieleza Dkt Kanenda. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Afya ya figo kwa wote, kuendeleza usawa katika ufikaji wa huduma na matumizi bora ya dawa” Dkt Kanenda akiitaka serikali kuyaingiza matibabu ya figo katika mfumo wa bima ya Afya ili kuwasaidia wagonjwa wanaopitia changamoto hiyo kufanyiwa upandikizaji kirahisi na kuokoa gharama za kufanya uchujaji damu. Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika, Dar es Salaam. #figo #matibabu #gharama #wagonjwa #ushauri #hospitali #bugando #muhimibili