Tume ya kitaifa ya uwiano na utangamano NCIC imewataka wanasiasa katika eneo la Bonde la Kerio kuwa mstari wa mbele kuhubiri amani miongoni mwa jamii zinazoishi katika maeneo ya mipakani. Tume hiyo imesisitiza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kukwepa matamshi ya chuki na badala yake kuhimiza mshikamano, hasa katika maeneo ambayo mara kwa mara hushuhudia migogoro inayotokana na wizi au mizozo ya mifugo.
Wakizungumza katika mkutano na wanahabari ulioandaliwa kuwahamasisha wanahabari kuhusu mbinu mwafaka za kuripoti visa vya uhalifu na mizozo katika eneo hilo, NCIC kwa ushirikiano na shirika la FPFK wamesisitiza umuhimu wa uandishi wa habari unaozingatia ukweli na unaochochea amani, wakisema wanahabari wana jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa wanazoripoti haziendelezi mivutano bali zinasaidia jamii kuelewa hali halisi na kutafuta suluhu.