Wafugaji katika Kaunti ya Kajiado wanalalamika kuhusu kupungua kwa biashara ya mifugo kufuatia mzozo unaoendelea katika mataifa ya Ghuba kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Kwa sasa, wafugaji ambao bado wanajikwamua kutokana na ukame uliodumu kwa miezi kadhaa wanasema biashara ya nyama imedorora pakubwa baada ya uuzaji na usafirishaji wa nyama kwenda Mashariki ya Kati kusitishwa.
Katika soko la Ilbisil, kumeshuhudiwa ongezeko la idadi ya mifugo wanaoletwa kuuzwa huku wanunuzi wakiwa wachache. Hali hii imesababisha kushuka kwa bei ya mifugo, jambo linalowasikitisha wafugaji.
Wafugaji wanasema mzozo huo wa Mashariki ya Kati sasa unasababisha hasara hasa kwa wale waliokuwa wamenunua mifugo kutoka Tanzania wakitarajia kuuza katika soko la kimataifa. Sasa wanaitaka serikali kurejesha mpango wa ununuzi wa mifugo kupitia Tume ya kitaifa ya Nyama, KMC ili kuwasaidia kukabiliana na hasara wanayopata.