Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola inaongezeka zaidi ya juhudi za kuudhibiti. Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya visa 900 vimeripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda, huku idadi ya waliofariki ikifikia watu 220. Visa viwili vipya vimeripotiwa nchini Uganda, na kufanya jumla ya wagonjwa kufikia saba nchini humo. Mkutano wa dharura umefanyika kwa njia ya kidijitali kati ya maafisa wa WHO na washirika wake ili kutafuta mbinu za kuzuia maambukizi zaidi, pamoja na kuimarisha ukaguzi katika mipaka na viwanja vya ndege.