Baada ya runinga ya Citizen kuangazia kisa cha Ruth Akiru, mwanafunzi kutoka familia maskini aliyefanya vyema katika mtihani wa Gredi ya Tisa lakini akashindwa kujiunga na sekondari ya juu kutokana na ukosefu wa karo,sasa tabasamu imerejea usoni mwake. Hatimaye, Ruth amejiunga na Shule ya Kitaifa ya Tartar baada ya Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, kumpatia ufadhili wa masomo.
Ruth Akiru anatoka katika makazi duni ya ADC Japata, Kaunti Ndogo ya Endebess. Kupitia ufadhili huo, Hatakua na wasiwasi wa karo hadi atakapokamilisha masomo ya chuo kikuu, ndoto iliyokuwa ikionekana mbali sasa ikipata mwanga. Kisa cha Akiru ni kielelezo cha changamoto zinazowakumba maelfu ya wanafunzi nchini wanaokabiliwa na ugumu wa kiuchumi katika kuendeleza masomo yao.