Wafanyabiashara katika Soko la Ishiara, Kaunti Ndogo ya Mbeere Kaskazini, wanaiomba serikali kuharakisha ufunguzi rasmi wa soko jipya la kisasa ambalo tayari limekamilika.
Wafanyabiashara hao wanasema soko hilo la ghorofa mbili limekamilika na vibanda vya biashara vimewekwa tayari kwa matumizi, lakini bado halijaanza kutumika rasmi. Mwenyekiti wa Soko la Ishiara, Gabriel Njue, amesema kukamilika kwa soko hilo ni afueni kubwa kwa wafanyabiashara ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya biashara chini ya jua kali na wakati mwingine kusitisha shughuli zao mvua inaponyesha.