Serikali ya kaunti ya Nyamira imetia sahihi mkataba wa makubaliano na shirika moja lisilo la kiserikali la` Lwala, ili kuwapa wahudumu wa afya nyanjani mafunzo ya kukabiliana na vifo vya kina mama wanapojifungua kwenye hospitali za umma katika kaunti ya hiyo.
Akiwahutubia wanahabari baada ya utiaji sahihi mkataba huo, afisa mkuu mtendaji wa shirika hilo Julius Mbea amesema shirika hilo linalenga kuleta vifaa maalum vitakavyotumika kupunguza visa vya kina mama kuvuja damu hadi kufariki wanapojifungua. Gavana Amos Nyaribo kwa upande amesema serikali yake itashirikiana kikamilifu na shirika hilo kuona kuwa mpango huo wa miaka mitano unafaulu. Kaunti ya Nyamira inalenga kupunguza vifo vya kina mama kutoka 349 hadi chini ya 100 kati ya 100,000 wanaojifungua katika kaunti hiyo kila mwaka