Zaidi ya watu 400 walemavu katika Kaunti ya Baringo wamenufaika na msaada wa viti vya magurudumu na vifaa vingine kupitia mpango wa siku tatu wa kuwafikia wananchi unaoendeshwa na shirika la Hope Mobility.
Mpango huo unalenga kurejesha matumaini, hadhi na kuboresha uhamaji wa watu wanaokabiliwa na changamoto za ulemavu katika maeneo mbalimbali ya kaunti. Kaunti ya Baringo inaendelea kurekodi idadi kubwa ya watu wanaoishi na ulemavu, hali inayochangiwa na kuumwa na nyoka, mashambulizi ya mamba, majeraha yatokanayo na mapigano na mashambulizi ya maara kwa mara, pamoja na magonjwa ya mtindo wa maisha na watoto wenye ugonjwa wa kupooza kwa ubongo. Maeneo ya karibu na Ziwa Baringo, pamoja na kaunti ndogo za Baringo Kaskazini na Kusini, yameathirika zaidi.