Wakulima wa viazi nchini wamekuwa wakipata mapato duni kutokana na wadudu waharibifu na gharama ya juu ya uzalishaji. Hata hivyo, watafiti wanatazamia kuwa mbinu za kisayansi zitawasaidia kubadili hali hiyo na kuongeza mavuno maradufu. Kilimo cha viazi vinavyostahimili ugonjwa sugu wa ukungu, ambao ndio changamoto kubwa zaidi kwa zao hilo, tayari kimeleta matumaini kwa wakulima wa viazi mjini Njoro, Kaunti ya Nakuru. Japo viazi hivyo vinaweza kuongeza utoshelevu wa chakula nchini, mafanikio yake yatategemea uhamasisho wa wakulima na idhini ya kisheria kuhusu matumizi ya vyakula vilivyoboreshwa vinasaba.