Baadhi ya viongozi wa kidini katika Kaunti ya Nandi, wakishirikiana na wadau mbalimbali, wametoa wito wa dharura kwa Serikali Kuu kuongeza mgao wa fedha wa kukabiliana na njaa nchini. Viongozi hao wanataka kuwepo kwa mikakati thabiti ya kusaidia zaidi ya Wakenya milioni tatu ambao kwa sasa wanakabiliwa na makali ya ukame katika kaunti 23 kote nchini.
Wakizungumza katika eneo bunge la Emgwen wakati wa ibada maalum ya shukrani, viongozi hao walipongeza mamia ya Wakristo waliojitolea kuchangia msaada wa chakula kwa shule ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia ya Kapsabet. Akiongoza hafla hiyo, Askofu wa Kanisa la AIC Jimbo la Nandi, Moses Serem, alisisitiza kuwa hali ya usalama wa chakula bado ni tete huku akibainisha kuwa juhudi za jamii pekee hazitoshi kukabiliana na janga hili ambalo limekithiri tangu mwaka jana.