Wakazi katika kaunti ya Murang’a sasa wanaitaka serikali ya kaunti kuweka bajeti maalum kwa ajili ya kununua magari zaidi ya kuzima moto na kujenga vituo vya zima moto katika kaunti ndogo zote huko Murang'a.
Wito huo umetolewa kufuatia kuongezeka kwa matukio ya moto ambayo yamesababisha hasara kubwa ya mali na kuacha baadhi ya familia bila makazi.
Wakizungumza katika eneo la Gakui, Eneo bunge la Kandara, wakazi pamoja na viongozi wanasema kuwa katika siku za hivi karibuni, visa vya moto vimeongezeka kwa kiwango kinachowatia wasiwasi. Wanalalamikia ukosefu wa vituo vya kutosha vya zimamoto wakisema hali hiyo imekuwa ikichangia kuchelewa kwa huduma za dharura, mikasa ya moto inapotokea.