Jumla ya ajali 6,685 ziliripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku watu 1,359 wakipoteza maisha na wengine zaidi ya elfu tatu kupata majeraha mabaya.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi, NTSA, vifo hivyo vinaashiria ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Watembea kwa miguu ndio walioathirika zaidi, huku watu 484 wakipoteza maisha katika ajali za barabarani.
Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa madereva 120 walifariki, huku abiria 245 wakipoteza maisha.
Aidha, waendeshaji wa pikipiki, maarufu kama boda boda, 362 walifariki katika ajali, huku watu 16 waliokuwa wakiendesha baiskeli wakipoteza maisha.
Kwa upande mwingine, watu 2,200 waliripotiwa kupata majeraha madogo kutokana na ajali hizo.