Timu ya taifa ya kandanda ya wanawake ya chini ya miaka 17 itachuana na Uganda katika mechi ya raundi ya pili ya kufuzu kwa Kombe la Dunia. Uganda itakuwa mwenyeji wa mkondo wa kwanza mnamo Mei 22, huku mechi ya marudiano ikichezwa tarehe 30 Mei katika Uwanja wa Nyayo.
Nyota hao wanakutana na Uganda wakiwa na ujasiri baada ya ushindi wa jumla wa mabao 7-1 dhidi ya Namibia katika raundi ya kwanza. Uganda pia wana msukumo baada ya kuingia raundi ya pili kwa ushindi wa 6-1 dhidi ya Zimbabwe. Kenya itakuwa ikitafuta nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya pili.
Mshindi wa mechi kati ya Kenya na Uganda atamenyana na Cameroon katika raundi ya tatu na ya mwisho ya kufuzu. Cameroon, Nigeria, Guinea na Zambia tayari zimefuzu kwa raundi ya mwisho ya mechi hizo za kutafuta wawakilishi kutoka Afrika.