Kutofahamu kuhusu karo ya vyuo vikuu kumewaweka wanafunzi kwenye njia panda, huku walioripoti vyuoni kwa mwaka wa kwanza wakikosa kufahamu kiwango cha karo wanachopaswa kulipa.
Hali hiyo imewasababishia dhiki, kwani hata mikopo na ufadhili wanaopaswa kupata kutoka kwa serikali bado hawajatumiwa, huku mustakabali wao ukiwa haujulikani.
Haya ni baada ya Wizara ya Elimu kuwaagiza wanafunzi kuripoti vyuoni wakisubiri mfumo mpya wa ufadhili wa masomo, ambao bado haujajadiliwa na kuidhinishwa na Bunge.
Mkanganyiko huo pia unawapa wazazi tumbo joto, kwani baadhi ya vyuo vinahitaji kiasi fulani cha pesa ili kuwasajili wanafunzi.