Wakulima wa maembe katika Kaunti ya Embu wanatarajiwa kunufaika na kukamilika kwa soko la kisasa la Karurumo katika eneo bunge la Runyenjes. Mradi huo wa shilingi milioni 60 unalenga kupunguza hasara kwa wakulima wa maembe baada ya mavuno.
Wakulima wa kaunti ya Embu ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa maembe nchini, lakini wamekuwa wakipata hasara kutokana na ukosefu wa masoko na vifaa vya kuhifadhi mazao yao. Soko hilo jipya litakuwa na majokofu na maeneo ya kuhifadhi mazao, hatua itakayosaidia kuhifadhi maembe na kuongeza bei sokoni. Mwenyekiti wa soko hilo, Joseph Njagi, alisema wakulima wamekuwa wakipoteza mazao mengi na kupata hasara. Soko la Karurumo ni miongoni mwa masoko 12 yanayojengwa katika kaunti ya Embu ili kuimarisha kilimo.