Vijana, wafanyibiashara pamoja na wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi wamelalamikia uhaba mkubwa wa nafasi za kazi wakisema hali hiyo imeendelea kuwa kizingiti kikuu kwa maendeleo ya eneo hilo. Wakizungumza mjini Kapenguria wakati wa kikao cha jopo la Okiya Omtatah cha kukusanya maoni kuhusu jinsi taifa linafaa kuendeshwa,
wananchi wamesema Kaunti ya West Pokot ni miongoni mwa maeneo yaliyosalia nyuma kwa muda mrefu kutokana na ukosefu wa uwekezaji, viwanda na fursa za ajira. Aidha wameitaka serikali kuu pamoja na serikali ya kaunti kuweka mikakati maalum ya kuimarisha elimu ya kiufundi, kusaidia biashara ndogo ndogo na kuvutia wawekezaji ili kupunguza ukosefu wa ajira. Kadhalika, wananchi hao wamesisitiza kuwa eneo hilo linahitaji kupewa uangalizi maalum na serikali kutokana na changamoto za kihistoria zinazokwamisha maendeleo, wakisema wakazi wengi wana uwezo na bidii lakini hawapati fursa za kuinua maisha yao kiuchumi.