Huku ujenzi wa barabara ya Tarbaj hadi Kutulo ukiendelea, mradi huu unaonekana kuleta manufaa zaidi kwa kutimiza mahitaji ya kimsingi ya jamii zinazoishi maeneo hayo.
Kampuni ya ujenzi ya Halane inayotekeleza ujenzi huo chini ya mradi wa Horn of Africa Gateway Development , imetoa msaada wa chakula cha iftar kwa familia zinazoishi kando ya mradi huo.
Msaada huo uliosambazwa katika maeneo manne umenufaisha zaidi ya familia 200 zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na maji, huku Waislamu wakiendelea na ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kampuni hiyo pia imechimba visima katika eneo hilo ili kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa wakazi.