Maiti moja imepatikana kutoka kwenye jengo la ghorofa nane lililoporomoka katika eneo la Olenairi, Oloolua, Kajiado Kaskazini, huku juhudi za kuwatafuta watu wengine watatu zikiingia siku ya tatu.
Naibu Kamishna wa Kajiado Kaskazini, Yusuf Mohammad, amesema shughuli za uokoaji zimetatizwa baada ya sehemu nyingine ya jengo hilo kuonyesha dalili za kuporomoka. Kutokana na hali hiyo, sehemu nyingine ya jengo hilo imebomolewa kimakusudi ili kuwapa nafasi maafisa wa uokoaji kuendelea na shughuli zao. Operesheni ya kusaka watu zaidi waliokwama inaendelea.