Baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Nyamira wamelalamikia idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kujisajili kuwa wapiga kura katika kaunti hiyo. Aidha wamewarai vijana kujisajili kwa wingi ili kuchukua nafasi yao ya kidemokrasia kushiriki katika kuwachagua viongozi wao.
Wakizungumza katika eneo bunge la Kitutu Masaba walipohudhuria hafla mbalimbali, viongozi hao wamewashauri vijana kutosalia nyumbani bila kujisajili kuwa wapiga kura. Naibu mwenyekiti wa chama cha Wiper Victor Swanya hata hivyo ameibua madai ya uwepo wa hitilafu za kimitambo ya KIEMS KITS na ukosefu wa vitambulisho, hali anayodai inahujumu zoezi la kuwasajili wapiga kura kwa wingi. Ameinyoshea serikali kidole cha lawama kwa madai ya kuhujumu zoezi hilo, kwa kutowashughulikia vijana waliojosajili kupata vitambulisho tangu mwezi Septemba mwaka 2025.