Wakazi wa eneo la Kabwareng katika eneo bunge la Aldai, Kaunti ya Nandi, wamejitolea kusaidia familia zisizojiweza kwa kuwajengea makazi ya heshima katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka.
Kundi hilo lililojumuisha viongozi wa kijamii, wafanyabiashara na vijana wa eneo hilo, lilikusanya rasilimali na kufanikisha ugawaji wa mabati kwa zaidi ya familia 200 ambazo zimekuwa zikiishi katika hali ya umaskini. Lengo lao ni kuboresha maisha ya familia hizo kwa kuwapa makazi salama na yenye heshima. Wengi wa walionufaika wamekuwa wakiishi katika vibanda visivyo imara, hali ambayo imekuwa ikichangia kusambaa kwa magonjwa hasa wakati wa mvua na baridi kali.