Wazazi wametakiwa kuichukulia likizo fupi ya Aprili kama nafasi muhimu ya kujenga uhusiano na watoto wao pamoja na kugundua na kuendeleza vipaji walivyonavyo. Wataalamu wa elimu wanasisitiza kuwa mchango wa wazazi nyumbani ni nguzo kuu ya kufanikisha utekelezaji wa mtaala wa CBE unaolenga kukuza uwezo binafsi wa mwanafunzi.
Wakizungumza katika kongamano la elimu katika Shule ya Kiungani Comprehensive, wadau wa elimu kutoka kaunti ya Trans Nzoia wamelalamikia tabia ya baadhi ya wazazi kuwaacha watoto wao wakitumia likizo kwa kuzurura au kuwatembelea marafiki bila uangalizi wa karibu. Wanasema hali hii hupunguza nafasi ya wazazi kugundua mapema vipaji vya watoto na kuwalea ipasavyo. Wadau hao pia wamepongeza mtaala wa CBE wakisema unatoa mwanya mpana kwa wanafunzi kukuza talanta zao katika sekta tofauti. Hata hivyo, wameweka wazi kuwa mafanikio yake yatategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu ili kuhakikisha watoto wanapata manufaa kamili.