Gavana wa Kericho, Dkt Erick Mutai ametaka kufutiliwa mbali kwa hati miliki za ardhi zilizotolewa kwa njia zinazotiliwa shaka katika eneo la Chelimo Kevoko.
Gavana huyo ameiomba wizara ya ardhi kubatilisha hati hizo, huku pia akiwasilisha malalamiko kwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi kuchunguza mchakato wa ugawaji wa ardhi hiyo.
Kulingana na Mutai, ekari 155 za ardhi ambazo awali zilitengwa kwa ajili ya kuwahamisha takriban watu 1,500 waliokuwa wamekaa bila umiliki rasmi, zinadaiwa kugawiwa visivyo kwa wanasiasa, Wajumbe wa Bunge la Kaunti, na maafisa waandamizi serikalini. Inadaiwa pia kuwa baadhi yao walijipatia zaidi ya kiwanja kimoja kupitia udanganyifu wa orodha ya wanufaika. Gavana huyo alieleza kuwa ardhi hiyo ni sehemu ya eneo la ekari 800 lililotengwa kwa upanuzi wa mji wa Kericho, lakini lengo hilo lilivurugwa na vitendo hivyo vinavyodaiwa kuwa vya ufisadi.