Utawala wa kitaifa katika eneo la Kiriari, eneo bunge la Manyatta kaunti ya Embu umeanza kutekeleza hatua mpya za kukabiliana na mimba za utotoni huku viongozi wa kanisa wakionya kuhusu ongezeko la visa hivyo.
Chifu wa eneo hilo, Ephantus Njiru, ameeleza kuwa hatua za awali zilizokuwa zikiwalenga wavulana pekee hazijafanikiwa kudhibiti hali hiyo. Amesema sasa vyombo vya madola vitachukua hatua za kisheria dhidi ya wavulana na wasichana wanaohusika na mimba za utotoni, akitaja kesi ya hivi karibuni ambapo vijana walipelekwa mahakamani, wakatozwa faini na kuachiliwa huru kama sehemu ya mkakati huo mipya ya kumaliza jinamizi hilo.
Amewataka wazazi kuwajibika zaidi wakati wa likizo, akisema kuwa uzembe wa malezi unachangia tatizo hilo.