Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini (KEMRI) imepiga hatua katika utafiti wa tiba asilia baada ya kutambua zaidi ya aina 141 za miti ya dawa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet. Utafiti huu unalenga kutoa ushahidi wa kisayansi kwamba dawa za kienyeji zinaweza kutibu magonjwa ambayo yamekuwa changamoto kwa muda mrefu.
Hatua hii inaambatana na wito wa hivi karibuni wa Shirika la Afya Duniani wa kuhimiza ujumuishaji wa dawa za kienyeji katika mifumo ya utoaji wa huduma za afya kote ulimwenguni. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KEMRI, Profesa Elijah Songok, amesisitiza kuwa lengo kuu la utafiti huu ni kuthibitisha uwezo wa miti shamba kutibu magonjwa sugu. Chini ya mpango huu madaktari wa kienyeji na wakulima watahusishwa kikamilifu ambapo Serikali ya kaunti itawapa wakulima miche ya mimea hiyo ya dawa iliyotambuliwa ili kuhakikisha upatikanaji endelevu.