Waziri wa Elimu, Julius Migos Ogamba, amewaonya walimu wakuu wanaokiuka mwongozo wa karo uliotolewa na serikali na kuwaongezea wazazi mzigo wa karo bila idhini ya wizara hiyo. Akizungumza kufuatia sakata ya karo ya zaidi ya shilingi 120,000 inayotozwa na Shule ya Upili ya Wasichana ya Alliance, Ogamba amesema kuwa wizara hiyo inachunguza malalamishi ya wazazi na wadau wengine kuhusu shule zaidi zinazotoza karo ya juu ili kuwachukulia wasimamizi na bodi za shule hizo hatua. Sakata hilo la karo limesababisha bodi ya shule ya Wasichana ya Alliance kubanduliwa huku TSC ikiagizwa kumchukulia mwalimu mkuu hatua kali.