Kamishna wa Kaunti ya Trans Nzoia, Gideon Oyagi, ametoa onyo kali kwa magenge na wahalifu wanaohangaisha wakazi wa eneo hilo, akiwataka wajisalimishe mara moja kabla mkono wa sheria haujawafikia.
Haya yanajiri huku idadi ya washukiwa waliokamatwa ikifikia 226 ndani ya kipindi cha chini ya wiki moja tangu kuanza kwa oparesheni maalum ya kusaka magenge katika kaunti hiyo. Aidha, polisi wamefanikiwa kurejesha mali mbalimbali zinazoshukiwa kuibwa na wahalifu hao wakati wa msako huo. Oyagi amesisitiza kuwa oparesheni hiyo itaendelea bila kusita hadi wahalifu wote watakapotiwa mbaroni. Aidha, amewataka viongozi na wanasiasa kushirikiana na vyombo vya usalama bila kuingiza siasa, ili kuhakikisha eneo hilo linarejea katika hali ya utulivu na usalama wa kudumu. Wiki iliyopita, vyombo vya usalama vilianzisha oparesheni hiyo maalum ya kusaka magenge ya vijana yanayotumiwa kuhangaisha wakazi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na ongezeko la uhalifu na kurejesha amani katika jamii.