Mamia ya wakazi wa Kijiji cha Mukamini, eneo la Bamba kaunti ya Kilifi wanaishi kwa hofu ya kufurushwa baada ya kubainika kwamba zaidi ya ekari 10,000 za ardhi yao ya jamii zinauzwa kwa njia tatanishi.
Wakaazi hao waliotoa malalamishi yao katika mkutano wa faragha huko Bamba walidai kuwa kamati ya zamani ya ardhi eneo hilo, kwa ushirikiano na baadhi ya maafisa wa serikali, inauza sehemu ya ardhi ya jamii katika maeneo ya Mnagoni na Mapotea bila kuhusisha wananchi. Viongozi wa serikali kuu wakiongozwa na Katibu wa Vijana Fikirini Jacobs, walihudhuria mkutano huo na kuthibitisha kwamba malalamishi hayo ni ya kweli na kuahidi kuchukua hatua za kisheria.