Wataalamu wa maswala ya afya nchini wameitaka jamii kuzingatia umuhimu wa kufanyiwa vipimo vya kimatibabu mara kwa mara. Wameonya kuwa magonjwa mengi yanayowakabili wananchi yanaweza kudhibitiwa vizuri na kupona endapo yatagunduliwa katika hatua za mwanzo kabla ya kuwa makubwa.
Wameibua wasiwasi mkubwa kuhusu tabia inayoenea ya watu kutumia dawa bila ushauri wa daktari, ambapo wengi huchagua dawa za dukani badala ya kwenda hospitali kupata ushauri wa kitaalamu. Wakizungumza katika zoezi la kutoa huduma za afya lililofanyika Kangema, maafisa hao walibainisha kuwa saratani, kisukari na shinikizo la damu ndio magonjwa yanayowatesa zaidi wakazi wa eneo hilo, na kusisitiza haja ya uchunguzi wa kila mara.