Serikali ya kitaifa imesisitiza dhamira yake ya kulinda maisha na vyanzo vya riziki huku maeneo kadhaa ya nchi yakiendelea kukumbwa na hali ya ukame.
Wakiongozwa na maafisa wa Idara ya Huduma Za Umma, viongozi hao wamefanya ziara ya kutathmini hali ya Ukame katika eneo la Wajir Mashariki ili kujionea athari za ukame na kusimamia zoezi la ugawaji chakula cha msaada.
Idara hiyo imesema juhudi za kukabiliana na ukame zinaongozwa na takwimu sahihi ili kuhakikisha misaada inawafikia waliokusudiwa. Kufikia sasa, serikali imesambaza magunia ya mchele na maharagwe katika kaunti ya Wajir ambapo kaunti ndogo 15 zimeathirika. Licha ya baadhi ya maeneo kuingia katika awamu ya tahadhari ya ukame, serikali imethibitisha kuwa hakuna kifo cha binadamu kilichoripotiwa, huku hatua kama usambazaji wa maji kwa magari na ulinzi wa mifugo zikiendelea kuwekwa..