Serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali imezindua rasmi mpango wa usafirishaji maji kwa malori unaolenga jamii zilizoathirika zaidi na ukame na uhaba mkubwa wa maji katika kaunti ndogo sita za Kaunti ya Wajir.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo unaodhaminiwa na Baitul-Maal Kenya, Mwenyekiti wa Mamlaka ya Masoko ya Mtaji nchini, Ugas Sheikh Mohammed, alisema hatua hiyo inalenga kufikia maeneo kadhaa yaliyoathirika pakubwa ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya kaya, mifugo, pamoja na makundi yaliyo hatarini ambayo maisha yao ya kila siku yanategemea rasilimali hiyo muhimu.