Wadau wa mazingira katika Kaunti ya Kilifi wamezitaka jamii zinazoishi katika maeneo ya mabwawa na pwani kuipa kipaumbele uhifadhi na upandaji wa mikoko ili kusaidia kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda mfumo wa ikolojia ya bahari.
Wakizungumza wakati wa hafla ya uhamasishaji katika eneo la Kidundu-Mkongani, maafisa kutoka Mamlaka ya Masuala ya Bahari nchini (KMA) wamesema kuwa urejeshaji wa mikoko ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kulinda viumbe wa majini na kupunguza uharibifu wa maeneo ya pwani.